Familia ya dereva wa benki ya CRDB Tawi la Ifakara, Dustan Rwegasira
(31) juzi ilifanya ibada ya mazishi kando kando ya Mto Kilombero bila ya
kuwapo kwa mwili wa ndugu yao huyo, ambaye hakuonekana kwa siku 10
tangu azame mtoni humo kufuatia ajali ya kivuko.
Kabla ya mazishi hayo, palitangulia ibada ambayo ilifanyika nyumbani kwa wazazi wa 'marehemu', mtaa wa Nyamvisi kata ya Ruaha.
Kivuko cha MV II Kilombero kilizama katika Mto Kilombero Januari 27
kikiwa na abiaria na mizigo, kutokana na kusukumwa hovyo na upepo mkali.
Ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa Benki ya CRDB walikusanyika saa
nane mchana kando kando ya mto huo, wakiongozwa na baba mzazi, Francis
Rwegasira.
Wengine walioshiriki mazishi hayo ni mkewe Flora Hamadi na baba mkubwa
Melchior Muangi. Walitupia majini sanda na baadhi ya nguo za marehemu.
Ndugu hao, jamaa na mafariki walichota pia mchanga kando kando ya mto
huo na kuumwaga kwenye maji ikiwa ni sehemu ya mila za kabila la wahaya.
Muangi alisema Serikali inapaswa kuwa na vifaa maalumu vya kupimia hali
ya hewa katika maeneo ya vivuko ili kunusuru majanga zaidi yanayoweza
kuepukika, kama ambalo limewafanya kumpoteza Rwegasira.
Wakati huo huo, zoezi la kukinasua kivuko cha MV II Kilombero
kilichopinduka katika Mto Kilombero tangu Januari 27, linaendelea vyema
ambapo sasa kionekana kuibuka nusu.
Mkuu wa kikosi cha uzamiaji na uokoaji kutoka kampuni ya M. Divers Ltd
ya Dar es Salaam, Hafidh Seif alisema wamezamisha matanki mawili ya lita
5,000 kila moja na kuyafunga kwa nyaya chini ya kivuko na maji
yaliondolewa kwa upepo na kufanya kivuko kilichokuwa kimezama kuibuka
nusu.
Alisema wameongeza matanki tisa ya lita 2,000 na 3,000 wakiamini ni lazima kitaibuka chote.
Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi mkoa wa Morogoro (Temesa), Mhandisi
Magreth Mapela alitoa wito kwa wananchi kuwa na subira wakati watalaamu
wakifanya kazi ya kuibua kivuko hicho.
Alisema baada ya kuopolewa, kivuko kitachunguzwa kwa kina na wataalamu
ili kifanyiwe marekebisho na kurejeshwa majini kuendelea na kazi ya
kuvusha watu pamoja na mali zao wakati huu ambao daraja la Mto Kilombero
likiendelea kujengwa.
Mapela alisema kivuko hicho kikuubuka chote, watatumia magari matatu,
mawili yenye uzito wa tani 25 na jingine lenye uzito wa tani 35,
kukivuta kivuko hicho hadi eneo la nchi kavu.
No comments :
Post a Comment